Bingwa wa dunia wa masumbwi uzito wa Welterweight, Manny Pacquiao ameeleza anachoamini kuwa ni sababu ya mpiganaji wa Japan Tenshin Nasukawa kulia baada ya kupigwa na Mayweather, Desemba 31 mwaka jana.
Katika pambano hilo la maonesho lililokuwa na raundi tatu, Mayweather alimpiga kikatili Nasukawa akimdondosha mara tatu kwenye raundi ya kwanza na kusababisha timu ya mpiganaji huyo kurusha taulo ulingoni wakimaanisha kuomba kumalizika kwa pambano.
Akizungumza katika mahojiano ya kutangaza pambano kati yake na Andrien Broner litakalofanyika Januari 19, Pacquiao ameeleza kuwa alishangazwa na kilichotokea ulingoni kwani aliamini kuwa pambano hilo lilikuwa la maonesho na sio pambano halisi.
Alisema kuwa Nasukawa alilia baada ya kuona ameshushiwa kipigo kama pambano la kweli, wakati lilikuwa pambano la kufanya maonesho.
“Sisi kama mabondia tunafahamu nini maana ya pambano la maonesho. Kwenye pambano la maonesho ni kuonesha tu namna ya kupigana lakini sio kama mnapigana kama mnashindana, na hii ndio sababu uliona yule mvulana alikuwa analia,” alisema Manny Pacquiao.
“Kwenye pambano la maonesho hutakiwi kumzimisha mtu (knock out). Unatakiwa kuonesha tu kuwa unampiga lakini sio kwa kiasi kile. Yule kijana alilia kwa sababu hakutegemea kuwa atapigwa vile kwa sababu ni maonesho (exhibition match),” aliongeza.
Manny Pacquiao na Mayweather walipigana mwaka 2015, Mayweather akatangazwa mshindi baada ya raundi 12 za pambano hilo lililobatizwa jina la ‘Pambano la Karne’.
Katika mahojiano hayo, Pacquiao aliulizwa maswali na bondia maarufu, Shawn Porter.