Bondia Manny Pacquiao ameliomba Shirikisho la Masumbwi Duniani (WBO) kuanzisha uchunguzi maalum kuhusu matokeo ya pambano kati yake ya bondia wa Australia aliyemvua taji la ubingwa wa dunia, Jeff Horn.
Bondia huyo mwenye umri wa miaka 38 ambaye aliwahi kushinda ubingwa wa dunia katika uzito tofauti, alitoa tamko rasmi la maandishi akiunga mkono wito uliotolewa na Bodi ya michezo ya Ufilipino (Philippines’ Games and Amusement Board).
Bodi hiyo iliiomba WBO kufanya marejeo ya pambano hilo na kuwachukulia hatua za kinidhamu majaji na mwamuzi, endapo itajiridhisha kuwa matokeo yaliyotangazwa hayakuwa na uhalisia kama wanavyoamini.
“Ninapenda mchezo wa masumbwi, sitaki kuuona ukakufa kwa sababu ya maamuzi yasiyo ya haki,” ameandika Pacquiao. “Nilikuwa nimeshakubali matokeo lakini kama kiongozi na wakati huohuo kama mpiganaji, nina wajibu wa kusaidia kuhimiza ukweli, haki na uhalisia kwenye macho ya umma. WBO wanapaswa kuchukua hatua kuhusu barua waliyotumiwa na Bodi [ya Ufilipino,” aliongeza.
Pacquiao alisisitiza kuwa endapo ukweli utakaobainika utawatia hatiani mwamuzi na majaji watatu wa pambano hilo, wachukuliwe hatua kwani matokeo hayawezi kubatilishwa.
Hata hivyo, WBO wamejibu kupitia mtandao wa Twitter wakieleza kuwa kwa mujibu wa sheria za mchezo huo, hakuna hatua zozote zinazoweza kuchukuliwa kwa waamuzi au majaji wa pambano, au kuhusu matokeo husika, isipokuwa endapo kumekuwa na tuhuma za rushwa na uvunjifu wa sheria ambayo yote sio madai ya maombi yaliyowasilishwa.
WBO walieleza kuwa kwakuwa mkataba wa Pacquiao na Horn unaelekeza kuwepo pambano la marudiano, shirikisho hilo linaunga mkono pambano hilo la marudiano.
Pacquiao aliingiza kiasi cha dola za kimarekani milioni 10 ($10 million), na Horn alichukua dola laki tano ($500,000).
Matokeo ya pambano hilo yalionekana kupingwa na watu wengi zaidi, huku matokeo ya kielekroniki (Compubox) yakionesha kuwa Pacquiao alifikisha ngumi za wazi 182 huku Horn akifikisha 92. Kadhalika, ilionesha kuwa Horn alirusha ngumi nyingi zaidi lakini alifanikiwa kufikisha asilimia 15, huku Pacquiao akionekana kufikisha asilimia 32.