Padri wa Dayosisi ya Meaux nchini Ufaransa amesimamishwa kutoa huduma ya ubatizo na ndoa baada ya kusambaa kwa video inayomuonesha akimpiga kofi mtoto mdogo aliyekuwa analia wakati wa ubatizo.
Padri Jacque Lacroix mwenye umri wa miaka 89 ‘alimchapa’ kofi mtoto huyo baada ya kushindwa kuzuia hisia zake akikerwa na kitendo cha mtoto huyo kulia mfululizo kabla ya kumbatiza licha ya kumbembeleza akiwa mikononi mwake.
Video hiyo iliyotazamwa zaidi ya mara milioni 5 ndani ya muda mfupi kwenye YouTube inamuonesha padri Lacroix akimpiga kofi shavuni mtoto huyo mbele ya wazazi wake, hali iliyosababisha mwanamke aliyekuwa karibu naye kuingilia kati. Baadaye, mtumishi huyo wa kanisa aliwaomba radhi wazazi wa mtoto huyo.
Uongozi wa Dayosisi hiyo ulitoa tamko la kumsimamisha kazi Lacroix mwishoni mwa wiki ikilaani kitendo alichokifanya.
“Askofu Nahmias, Bishop of Meaux amemsimamisha kazi Lacroix na hataruhusiwa kushiriki katika huduma za ubatizo pamoja na ndoa. Hatua hii pia inamtaka kutojihusisha na masuala ya kanisa kwa sasa na atashiriki misa pale tu atakaporuhusiwa na mkuu wa Parokia,” limeeleza tamko hilo.
Padri Lacroix alifanya mahojiano na radio Info ya Ufaransa na kueleza kuwa alichofanya kwenye tukio hilo ilikuwa kati ya ‘kujali na kofi dogo’.
“Kilikuwa kitu ambacho kiko katikati ya kujali na kofi kidogo. Nilikuwa najaribu kumnyamazisha,” alisema.