Mamlaka ya Palestina imesema itaukaribisha msaada wa kimataifa katika uchunguzi wa kifo cha mwandishi wa habari wa Al Jazeera huku Israel ikisema itachunguza kuzuka kwa vurugu katika mazishi yake.
Kwa mujibu wa DW Polisi wa Israel walivamia na kuushambulia msafara wa waombolezaji wa Kipalestina, kwenye eneo la Mji Mkongwe waliokuwa wamebeba jeneza la mwandishi wa habari Shereen Abu Akleh, tukio ambalo limesababisha jumuiya ya kimataifa kulilaani.
Vurugu hizo ziliongeza hasira kwa Wapalestina baada ya mauwaji ya Shereen, ambayo yametishia kuchochea mivutano ambayo imekuwa ikiongezeka tangu Machi.
Waziri wa Usalama wa Ndani wa Israel Omer Barlev amesema kuwa yeye na kamishna wa Polisi wamekwishateua jopo la kufanya uchunguzi wa kina wa kile kilichotokea wakati wa mazishi na kwamba matokeo ya uchunguzi huo yatatolewa katika siku zijazo.
Mamlaka ya Palestina imekielezea kifo cha mwandishi huyo wa habari, ambaye alikuwa akiripoti uvamizi wa Israel katika eneo la Ukingo wa Magharibi linalokaliwa kwa mabavu kama tukio la mauaji la vikosi vya Israel.