Wabunge wa Kenya wanaotajwa kuwa kati ya wabunge wanaolipwa mishahara mizuri duniani wanakabiliwa na punguzo la mishahara yao.
Tume ya Mishahara na Stahiki ya Kenya (SRC) imeeleza kuwa inafanya mapitio mapya ya mishahara kwa lengo la kupunguza mzigo wa malipo kwa watumishi kwa asilimia 35.
Kutokana na mapitio hayo, wabunge wa nchi hiyo wanaopokea $7,200 kila mmoja kwa mwezi watakatwa asilimia 15 pamoja na kupunguziwa baadhi ya malupulupu yao. Mshahara wa mbunge hivi sasa utakuwa $6,100 huku malupulupu yake yakiwa chini ya kiwango alichozoea kupokea.
Aidha, BBC imeripoti kuwa marekebisho hayo mapya ya mishahara pia yataathiri mshahara wa Rais ambao umepunguzwa kutoka $16,000 hadi $14,000.
Panga la punguzo hilo pia litawagusa maafisa wengine wa ngazi za juu wa serikali.
Hivi karibuni, wabunge waliungana kupinga jaribio la kukatwa kodi kwenye mishahara yao kwa madai kuwa wananchi wa majimboni kwao wanawategemea kuwaomba misaada ya kifedha.
Kiongozi wa SRC amesema kuwa punguzo hilo la mishahara minono ni hatua nzuri ikiwa ni pamoja na hatua nzuri kwa kuondoa posho za kukaa kwenye vikao (sitting allowances).
Mishahara minono kwa wabunge wa Kenya imewahi kupingwa mara kadhaa na wanaharakati na wananchi wa nchi ambao kwa nyakati tofauti walikuwa wakifanya maandamano.