Ikulu ya Marekani (White House) imevamiwa na panya ambao wameonekana kuteka viunga vya Washington DC katika kipindi cha hivi karibuni.
Waandishi wa habari waliokuwa katika shughuli zao za kikazi ndani ya Ikulu wameeleza kuwa walishuhudia panya wanne wakikimbia kwenye makazi hayo ya Rais Donald Trump na kwamba panya mmoja mkorofi alipita juu ya mguu wa mwandishi wa habari.
John Robert, mwandishi wa habari wa kituo cha Fox, aliandika tweet akieleza namna ambavyo alikumbana na panya huyo mkubwa ambaye alipita juu ya mguu wake wa kushoto akiwa kwenye viunga vya White House.
So – I am standing in our @FoxNews standup location on the @WhiteHouse North Lawn and notice in my peripheral vision something moving at my left foot. I assumed it was one of the ubiquitous WH squirrels. But no….it was a big brown rat.
— John Roberts (@johnrobertsFox) December 17, 2018
Akizungumzia hali hiyo, Meneja wa Idara ya Afya ya Washington DC, Gerard Brown alisema kuwa panya hao walioonekana Ikulu ni sehemu ya panya wengi waliotoka kwenye maficho yao kutokana na mvua kubwa inayoendelea.
“Maji hayawezi kuwaua au hata kuwapunguza hata kidogo. Panya wanaweza kuogelea kwa muda hata wa wiki moja, lakini mvua inaweza kuwafanya kupata shida ya chakula. Hali inayowafanya watoke kwenye makazi yao kutafuta chakula,” Brown anakaririwa na Washington Post.
Alisema kuwa panya wanaonekana katika jiji hilo ni aina ambayo inaweza kuzaa watoto 10 ndani ya kipindi cha mwezi mmoja.
Ongezeko la panya linadaiwa kusababishwa na mvua pamoja na idadi kubwa ya watu walioongezeka katika viunga hivyo, hali inayomaanisha kuwepo kwa migahawa mingi na vyakula vinavyotupwa kama uchafu unaowavutia panya wengi.