Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Muliro Jumanne amesema jeshi la polisi limefanikiwa kudhibiti vikundi vya uhalifu maarufu kama panyaroad katika jiji hilo kwa asilimia 87.
Kamanda Muliro amebainisha hayo Oktoba 3, 2022 wakati wa mjadala kitaifa juu ya hali ya kiusalama na jitihada za Jeshi la Polisi katika kudhibiti panyarodi katika Mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Arusha na Dodoma ulioandaliwa na Watch Tanzania.
Kamanda Murilo amesema wanaendelea kufuatilia asilimia 13 ya vikundi vya uhalifu hasa kwa waliokimbia kwenye maeneo yao kwa kuwa lengo ni kufanikiwa kudhibiti vikundi hivyo kwa asilimia 100 hivyo bado wanaendelea kusaka wahalifu wengine katika jiji hilo.
Ameongeza kuwa miongoni mwa vijana 10 wanaokamatwa katika makundi hayo, watatu wanakuwa wametoka magerezani.
“Uko uhusiano wa karibu kati ya waliotoka magerezani na wahalifu hawa kwa sababu kati ya makundi tunayoyakamata na kuyapeleka mahakamani unakuta kwenye kundi kati ya watu 10 wamo watu watatu ambao wameshapita kwenye mifumo hii ya kisheria, Polisi, mahakamani wakaendaa mahabusu au magereza wakatoka kwa sababu mbalimbali za kisheria.”