Gwiji wa soka nchini Italia aliekua sehemu ya kikosi cha timu ya taifa ya nchi hiyo kilichotwaa ubingwa wa fainali za kombe la dunia mwaka 1982 zilizochezwa nchini Hispania, Paolo Rossi amefariki dunia.

Mke wa marehemu Federica Cappelletti ameweka picha ya mumewe na kuandika kwenye ukurasa wake wa Instagram, “Per Semper,” akimaanisha “Milele.”

Rossi aliefikwa na umauti akiwa na umri wa miaka 64, anaheshimika sana nchini Italia, kufuatia historia yake ya ya kutwaa tuzo ya Kiatu cha Dhahabu kwenye Fainali za Kombe la Dunia la mwaka 1982, baada ya kuibuka kinara wa ufungaji Bora.

Pia alitwaa tuzo ya Mpira wa Dhahabu kwa kutajwa kama mchezaji bora wa fainali hizo, na mwaka huo huo alitwaa tuzo ya mchezaji bora wa dunia (Ballon d’Or), na  mchezaji bora wa Ulaya.

Akiwa mchezaji wa mabingwa wa sasa wa Italia Juventus FC, Rossi alishinda mataji mawili ya Italia Serie A, Kombe la Uropa na Coppa Italia ndani ya miaka minane aliowatumikia magwiji hao wa mjini Turin.

Klabu nyingine ambazo Rossi alizitumikia wakati wa uhai wake ni Como (1975–1976),  L.R. Vicenza (1976–1979), Perugia (1979–1980),  Juventus FC (1973–1975/1981–1985), AC Milan (1985–1986) na  Hellas Verona (1986–1987).

Upande wa timu ya taifa ya italia aliitumikia kuanzia mwaka 1977–1986 akifunga mabao 20 kwenye michezo 48.

Ni siku chache zimepita tangu Dunia ilipoomboleza kifo cha gwiji wa soka ulimwenguni Diego Maradona, Rossi anakuwa mkongwe wa pili anayejulikana kwa kushinda kombe la Dunia kuaga Dunia mwaka huu 2020.

Lema, familia yake wakimbilia Canada
Flick: Robert Lewandowski atakua 'FIT'