Kupitia ujumbe wa Pasaka unaoangazia matumaini, Papa Fraancis Jana Jumapili aliwasilisha maombi kwa ajili ya watu wa Ukraine na Russia, aliyapongeza mataifa ambayo yanawakaribisha wakimbizi na kuwataka Waisraeli na Wapalestina wanaoukumbwa na ongezeko la ghasia kuaminiana.
Papa Francis, pamoja na maskofu kadhaa na maelfu ya waumini, walisherekea misa ya Pasaka katika uwanja wa Mtakatifu Petro uliopambwa kwa maua, wakithibitisha imani ya Kikristo kwamba Yesu alifufuka kutoka kwa wafu siku chache baada ya kusulubiwa kwake.
Papa mwenye umri wa miaka 86, aliongoza sherehe kwa hotuba ya kawaida kuhusu maeneo yenye matatizo duniani akihimiza kuaminiana kati ya watu, watu na mataifa, akisema furaha ya Pasaka inaangazia giza.
Hata hivyo, Wanadiplomasia wa Ukraine wamekuwa wakilalamika kwamba hajatoa msimamo thabiti katika taarifa zake juu ya Russia na hasa Vladimir Putin wakati Vatican inajaribu kuepuka kuitenga Moscow.