Kiongozi wa kanisa katoliki duniani, Papa Francis amekataa kuonana na Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo aliyeko ziarani mjini Vatican.

Mamlaka za Vatican zimeeleza sababu ya kiongozi huyo kutoonana na Pompeo kuwa ni msimamo wake wa kukataa kuonana na wanasiasa wakati wa Kampeni za uchaguzi.

Hatua hiyo inaongeza hali ya mzozo wa kidiplomasia baada ya kauli ya Pompeo kuhusu China na Kanisa Katoliki.

Vatican ilimshutumu Pompeo kuwa anajaribu kutumia suala hilo kuvutia wapiga kura wa uchaguzi wa urais wa mwezi Novemba nchini Marekani.

Katika makala ya mwanzoni mwa mwezi Septemba, Pompeo alisema kanisa Katoliki linapoteza ”mamlaka yake ya kinidhamu” kwa kufanya makubaliano mapya na China kuhusu uteuzi wa maaskofu.

Rais Donald Trump anaungwa mkono na mashirika ya kidini ya kihafidhina na wapiga kura wa Kikatoliki wa kihafidhina, ambao wengine wanadhani Papa Francis ni mtu mwenye uhuru sana.

”Papa aliweka wazi kabisa kuwa wanasiasa hawatapokelewa katika kipindi cha uchaguzi. Hii ndio sababu,” Shirika la Habari la AFP linamkariri Kadinali Parolin.

Boateng amfuata Silvio Berlusconi
Mauaji ya wazee yapungua