Kiungo wa klabu ya Olympic Lyon ya Ufaransa Pape Cheikh Diop Gueye, ametangaza maamuzi ya kusubiri kuitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Hispania, na kulikacha taifa la Senegal, ambapo ndipo asili yake ilipo.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 21, ametangaza maamuzi hayo, huku kila shabiki wa soka nchini Senegal akipatwa na mshangao, kutokana na sifa za kuzaliwa kwenye taifa hilo la Afrika magharibi.
Diop alizaliwa mjini Dakar, na alihamia nchini Hispania akiwa na umri wa miaka 14, ambapo alikuzwa kisoka nchini humo hadi kufikia hatua ya kuitwa katika kikosi cha vijana chini ya umri wa miaka 18 mwaka 2015.
Kiungo huyo pia ameshazitumikia timu za taifa za vijana za Hispania chini ya umri wa miaka 19 na 21.
Hata hivyo uongozi wa shirikisho la soka nchini Senegal (FSF) uliwahi kujaribu kumshawishi akubali kurejea nyumbani na kuitumikia timu ya taifa ya nchi hiyo (Teranga Lions), lakini aliutaka uongozi huo kuwa na subra hadi atakajifikiria kwa kina.
“Nimewahi kushawishiwa na viongozi wa shirikisho la soka la Senegal, ili niichezee timu ya taifa, lakini nimefanya maamuzi ya kuendelea kuwa sehemu ya timu ya taifa ya vijana ya Hispania, hadi nitakapoitwa kwenye kikosi cha wakubwa. ” Diop ameliambia gazeti la michezo la Hispania (The Marca).
“Ni kweli, siwezi kusahau asili yangu ilipo, mimi ni msenegal, lakini ninajihisi furaha kuwa hapa Hispania na kucheza katika timu ya taifa.”
“Hispania wamenipa matunzo mazuri katika mchezo wa soka hadi nimefikia hatua hii, sina budi kulipa fadhila kulitumikia taifa hili, ninaamini kwa hatua hii niliyoichukua sitokua nimefanya dhambi yoyote.”
Kwa mujibu wa sheria za shirikisho la soka duniani FIFA, bado Diop ana nafasi ya kubadili maamuzi yake ya kuichezea timu ya taifa ya Senegal, kwani mpaka sasa hajawahi kuitumikia timu ya taifa ya wakubwa ya Hispania.