Kiungo wa Ihefu FC, Papy Kabamba Tshishimbi huenda asirejee tena uwanjani katika michezo yote iliyosalia msimu huu baada ya kutakiwa kupumzika kutokana na kufanyiwa upasuaji mkubwa wa goti.
Kocha msaidizi wa Ihefu, Zubery Katwila amesema ni bahati mbaya kwa kiungo huyo kutoka DR Congo kama mchezaji na wao na kama benchi la ufundi kwani bado walikuwa wanahitaji huduma yake.
“Kwa yeye kurudi msimu huu ni ngumu ndio maana tukaona ni vyema tumpe muda mwingi wa kupumzika ili arudi akiwa imara zaidi, hivyo tunararajia kuanzia sasa ataanza mazoezi mepesi mepesi tu.” amesema Katwila
Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Klabu hiyo, Zagalo Chalamila amesema baada ya Tshishimbi kufanyiwa upasuaji jijini Dar es Salaam aliomba kwenda kwao, hivyo kuanzia wiki hii atarudi nchini.
“Mwezi uliopita alituomba aende kwao kwa ajili ya kuangaliwa zaidi na kupatiwa matibabu nasi kama viongozi tulimpatia hiyo ruhusa hivyo tunamtarajia kurudi muda wowote kuungana na wenzake.” Amesema Zagalo