Moto mkubwa uliozuka umeteketeza jengo la kanisa kongwe la kihistoria la Kikatoliki linalojulikana kama ‘Notre-Dame jijini Paris nchini Ufaransa, saa chache zilizopita.

Paa la kanisa hilo lenye umri wa miaka 850 limeteketea lakini sehemu mbili za minara ya kengele zimeokolewa na kikosi cha zima moto, kwa mujibu wa taarifa za maafisa wa Serikali ya Ufaransa.

Kikosi cha kuzima moto kimefanya kazi kubwa ya kuzima moto huo ingawa nguvu ya moto imekuwa kubwa zaidi ndani ya muda mfupi.

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron ambaye alifika katika eneo hilo, amesema kuwa tukio hilo ni janga kubwa la kitaifa na kwamba yuko pamoja na waumini wa Kanisa Katoliki katika kipindi hiki kigumu.

Chanzo cha cha kuzuka moto  huo bado hakijajulikana, huku maafisa wakiendelea kufanya kazi ya uchunguzi wa awali.

Maafisa wanasema kuwa huenda sababu kuu inatokana na ukarabati uliokuwa unaendelea kutokana na ufa ulioonekana kwenye moja kati ya mawe ya jengo hilo, hali iliyosababisha hofu ya kupunguza uimara wake.

Polisi wamesema mmoja kati ya maafisa wa zima moto amejeruhiwa vibaya katika zoezi hilo.

Maelfu ya watu wamekusanyika kwenye mitaa lilipo jengo hilo wakishuhudia, huku baadhi yao wakitokwa na machozi na kuimba nyimbo za kumuomba Mungu, kwa mujibu wa BBC.

Mahakama yaanika pesa kiduchu alizobaki nazo R. Kelly Benki
Video: Vyama vya upinzani vyamvaa Spika, Benki ya dunia yakunwa na kasi ya Rais Magufuli