Klabu bingwa nchini Ufaransa Paris Saint-Germain (PSG) wamewasilisha ofa ya Euro milioni 270 sawa na Pauni 239 kwa ajili ya usajili wa kiungo mshambuliaji kutoka nchini Brazil na klabu ya Barcelona ya Hispania Philippe Coutinho Correia.
Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa na gazeti la Mundo Deportivo la nchini Hispania zimeeleza kuwa, tayari ofa hiyo imeshawasili Camp Nou yalipo makao makuu ya klabu ya FC Barcelona, na kinachosubiriwa ni jibu kutoka kwa viongozi wa klabu hiyo.
Hata hivyo taarifa nyingine zinadai kuwa, baadhi ya viongozi wa Barca, waimekataa ofa hiyo, kwa kutaka iongozwe na kufikia Euro milioni 400 sawa na Pauni milioni 353.
Wakati mvutano huo ukiripotiwa kuendelea miongoni mwa viongozi wa Barcelona, bado vyombo vya habari vinaendelea kusubiri kwa hamu jibu sahihi ambalo litapatikana baada ya vikao vya ndani.
Tangu alipojiunga na mabingwa hao wa Hispania msimu wa 2007/18 mwezi Januari, Coutinho amecheza michezo 22 na kufanikiwa kufunga mabao 10, huku akitoa pasi za mwisho sita.
Barcelona walimsajili Coutinho kwa ada ya Euro milioni 142 sawa na Pauni milioni 100, akitokea kwa majogoo wa jiji Liverpool.
Endapo Barcelona watakubali ofa iliyowafikia mezani, Coutinho ataweka rekodi ya kuwa mchezaji ghali zaidi duniani katika kipindi hiki, akimpiku mshambuliaji wa PSG Neymar Jr, ambaye anaendelea kushikilia rekodo hiyo kufuatia uhamisho wake uliogharimu kiasi cha Euro milioni 222.
Mipango ya usajili wa Coutinho kuelekea PSG imekuja kufuatia uwezekano wa kuondoka kwa Neymar ambaye anawindwa na mabingwa wa soka barani Ulaya Real Madrid, ambao wanamsaka mbadala wa Cristiano Ronaldo anayehusishwa na taarifa za kutaka kutimkia Juventus ya Italia.