Mabingwa wa soka nchini Ufaransa Paris Saint-Germain (PSG), wametenga kiasi cha Euro Milioni 70 kwa ajili ya usajili wa mshambuliaji kutoka nchini Gabon na klabu ya Borussia Dortmund Pierre-Emerick Aubameyang.
Mpango wa usajili wa mshambuliaji huyo unasukwa hivi sasa, ikiwa ni siku chache kabla ya kuanza kwa dirisha la usajili wa majira ya kiangazi ambapo klabu kadhaa zitaingia sokoni kwa ajili ya kuimarisha vikosi vyao.
Wakati PSG wakipanga mpango huo, mapema hii leo wamekanusha taarifa za zilizochapishwa na gazeti la Bild la Ujerumani zinazodai kuwa, mchezaji ambaye amefunga mabao 35 msimu huu, tayari amekutana na Mkurugenzi wa Soka wa PSG, Patrick Kluivert mjini Paris.
Aubameyang, mwenye umri wa miaka 27, atakuwa anaingiza Euro Milioni 14 kwa msimu endapo atatua PSG, pato ambalo ni mara mbili ya mshahara wake wa sasa.
Mshambuliaji huyo mzaliwa wa Ufaransa, amekua gumzo kwa muda mrefu katika harakati za usajili barani Ulaya, na inasemekana klabu nyingine kama Real Madrid, Liverpool, Man City na Man Utd zinaiwania saini yake.