Beki kutoka nchini Ivory Coast na klabu ya Singida Big Stars Pascal Serge Wawa ameweka wazi mmoja wa washambuliaji ambao anawaona wana kitu kikubwa kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara ni Fiston Mayele anayecheza katika kikosi cha Mabingwa Watetezi Young Africans.
Wawa amesema Mayele ni mshambuliaji ambaye kama beki unapokutana naye inabidi utumie akili kubwa kukabiliana naye kwa sababu amekamilika anapokuwa ndani ya uwanja akiitetea timu yake.
“Mayele ni mchezaji mwenye nguvu, spidi na analijua sana goli kwa hiyo kwenye kukabiliana naye lazima uwe na kitu cha ziada, ni mchezaji mzuri sana kwa washambuliaji ambao wapo kwenye ligi hapa,”
“Namwombea kwa Mungu aendelee kufanya vizuri atoke pale alipo na aende sehemu ambayo ataendelea kupata pesa nyingi ili familia yake izidi kujivunia kuhusu yeye.”
Wawa amesema alishawahi kukutana na mchezaji huyo nje ya uwanja alipokwenda kumtembelea mchezaji mwenzake wa Singida BS (Francis Kazadi) ambaye ni raia wa DR Congo.
“Nilikutana naye nje ya uwanja nilikuwa nyumbani kwa Kazadi wakati huo tulikuwa na mapumziko mafupi Dar, alinikuta pale alikuja kulikuwa na wenzake wengine, ni mchezaji ambaye ana utu sana;”
“Mchangamfu na tulipiga stori kama vile tunafahamiana kwa hiyo hata nje ya uwanja ni mtu mzuri kwa sababu tulikuwa kama watu ambao tunafahamiana kwa muda mrefu.”
Wawa amejiunga na Singida BS mwanzoni mwa msimu huu baada ya mkataba wake na Simba SC kumalizika.
Hata hivyo, pamoja na Wawa kusema hajawahi kukutana na Mayele uwanjani, kuna uwezekano mkubwa wakakutana sasa kwenye mchezo wa Nusu Fainali wa ASFC endapo Young Africans wataichapa Geita Gold FC kwenye Jumamosi (April 08) katika mchezo wa Robo Fainali na mchezo wa Ligi Kuu.