Mshambuliaji kutoka nchini Rwanda Meddie Kagere, leo asubuhi alikosa mazoezi ya kikosi cha mabingwa wa soka Tanzania bara wekundu Wa Msimbazi Simba.

Simba walirejea mazoezini jana jumatatu, baada ya kupumzika kwa siku mbili, kufuatia mchezo wa mzunguuko wa pili wa ligi kuu dhidi ya Mtibwa walioucheza siku ya ijumaa na kuibuka na ushindi wa mabao mawili kwa moja.

Katika hali ya kushangaza Kagere anaeongoza kwa mabao katika kikosi cha Simba hakuonekana, hali ambayo iliwapa nafasi waandishi wa habari kumuuliza kocha Aussems kulikoni?

Baada ya mazoezi ya kikosi hicho yaliyofanyika katika viwanja vya Gymkhana jijini Dar es salaam, kocha Patrick Aussems alijibu swali hilo.

Kocha huyo kutoka nchini Ubelgiji alisema Kagere anasumbuliwa na majeraha, hivyo alilazimika kumpumzisha.

“Kagere alipata majareha kidogo ndio maana nimeamua kumpumzisha, lakini inabidi nimuangalie zaidi,” alisema kocha Aussems.

Aussems alisema washambuliaji wake John Bocco na Wilker Da Silva bado hawajawa fiti kucheza, hivyo analazimika kumuangalia zaidi Kagere, ili asijikute akiwapoteza wote kwa pamoja.

Akizungumzia mshambuliaji wake Mbrazili Wilker Da Silva aliyerejea, alisema jambo zuri kwake katika kipindi hiki.

“Nafuahi kumuona akiwa ameanza mazoezi na wenzake kwa sababu ndio kitu ambacho nilikuwa nakitaka, nahitaji acheze.”

Simba SC tayari imeshacheza michezo miwili ya ligi kuu ya soka Tanzania bara msimu huu, na imefanikiwa kujikusanyia alama sita zinazoendelea kuwaweka kileleni mwa msimamo.

Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Septemba 18, 2019
Walioua kwa mil. 1, wahukumiwa kunyongwa hadi kufa