Baada ya kulazimisha matokeo ya sare ya bila kufungana dhidi ya Young Africans, Kocha Mkuu wa Maafande wa Magereza ‘Tanzania Prisons’ Patrick Odhiambo amefichuia siri ya kuambulia alama moja dhidi ya vinara hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Young Africans ikicheza nyumbani juzi Jumatatu (Mei 09), ilishindwa kufurukuta kwa Tanzania Prisons, huku Mshambuliaji wake kutoka DR Congo Fiston Kalala Mayele akikosa mkwaju wa Penati, kufuatia kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ kuangushwa eneo la hatari.

Kocha huyo kutoka nchini Kenya amesema siri kubwa ya kulazimisha sare dhidi ya Young Africans kwenye mchezo huo ilitokana na kujua namna ya kubana mashambulizi ya wapinzani wake.

Odhiambo amesema Young Africans imekua ikitumia upande wa kulia kupeleka mashambulizi kwa timu pinzani msimu huu, na beki wa upande huo Djuma Shaban amekua chagizo la kutimiza mpango huo.

“Young Africans inatumia zaidi upande wa Djuma (Shaban) na mimi kule niliwaweka wachezaji wawili ambao niliona kabisa wana nguvu ya kumzuia,”

“Alicheza Benjamin Asukile kama winga (nafasi yake ni beki) pamoja na Ibrahim Abraham na walikuwa kwenye maelewano makubwa ya kuubana upande ambao tulijua una madhara.”

Kocha Odhiambo pia akafichua siri nyingine iliyotumika kumakabili Mshambuliaji Fiston Mayele, ambaye katika mchezo huo alishindwa kuwafurahisha Mashabiki na Wanachama wa Young Africans.

“Kumbana Mayele Nilimuambia Chona (Nurdin) awe makini na Mayele kwa sababu akiwa ndani ya boksi hapo ndo anakuwa mzuri sana kwenye kufunga, aliweza kumbana kwa dakika zote.” amesema Odhiambo

Huenda mbinu za Kocha Odhiambo zikawa na faida kubwa kwa Kocha Mkuu wa Dodoma Jiji FC Masoud Djuma Irambona, ambaye mwishoni mwa juma hili (Mei 15) atakua na kazi ya kuikabili Young Africans Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.

Young Africans inaendelea kuongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 57, ikiiacha Simba SC kwa tofauti ya alama 11, huku nafasi ya tatu ikishikwa na Azam FC yenye alama 32.

Dodoma Jiji FC itakayocheza dhidi ya Young Africans Jumapili (Mei 15) ipo nafasi ya tisa, ikifikisha alama 27.

KMC FC kukiwasha na Mtibwa Sugar Uhuru Stadium
Hamis Kiiza: Simba SC imebadilika sana