Aliyekuwa nahodha na kiungo wa Arsenal, Patrick Vieira anaamini meneja wa klabu hiyo Arsene Wenger ataendelea kuwa mkuu wa benchi la ufundi, licha ya mustakabali wake kuwa kwenye hali ya sintofahamu.

Vieira ambaye kwa sasa ni meneja wa klabu ya New York City inayoshiriki ligi ya nchini Marekani, amesema Wenger ana nafasi kubwa ya kusaini mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia The Gunners, kutokana na mambo aliyoyafanya klabuni hapo tangu alipoajiriwa kwa mara ya kwanza mwaka 1996.

Vieria amesema kinachoendelea kufanywa na mashabiki wa Arsenal kwa kushinikiza meneja huyo asipewe mkataba mpya, ni sawa na kazi bure, kwani kuna uwezekano mkubwa kwa mzee huyo kutokuwa na makosa ya matokeo yanayokiandama kikosi cha The Gunners kwa sasa.

Amesema wachezaji wa Arsenal wanapaswa kuchunguzwa na kisha kulaumiwa kwa kile kinachoendelea klabuni hapo, kwani wao ndio wenye jukumu la kupambana kwa hali yoyote, ili timu ifanikiwe kupata ushindi na kisha kutwaa mataji.

“Nafahamu Arsene sio mtu wa kulaumiwa, kwa sababu kuna mapungufu makubwa ambayo yapo kwenye kikosi cha Arsenal ambayo yanapaswa kurekebishwa na wachezaji,”alisema.

“Nafahamu pamoja na joto la kutaka asipewe mkataba mpya kuendelea kupanda tangu walipofungwa mabao matano kwa moja dhidi ya Bayern Munich katika michezo ya nyumbani na ugenini, bado Wenger ataendelea kupambana ili afanikishe azma ya kukabidhiwa mkataba mpya, “aliongeza.

“Ni kweli mashabiki na wadau wengine wa soka wameonyesha kutokua na imani dhidi yake, lakini kwa upande mwingine uchunguzi unatakiwa kufanya kwa kuwaangalia wachezaji, ni vipi wanavyotimiza wajibu wa kupokea maagizo kutoka kwa meneja wao na kuyafanyia kazi, “alifafanua.

Kuhusu kitendo cha Wenger kumuweka benchi Alexis Sanchez kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Liverpool ambao walipata ushindi wa mabao matatu kwa moja, Vieira amesema kuna walakini ulijitokeza baina ya meneja huyo wa kifaransa na mchezaji husika.

Alisema anafikiri kuna wachezaji wanamuangusha Wenger na kwamba inapofikia hatua hiyo meneja ana wajibu wa kuchukua maamuzi yoyote kwa kuamua amchezeshe nani, na nani akae benchi kusubiri kuingia wakati atakapohitajika kwenda kutoa msaada.

“Mimi sikushangazwa na jambo hilo kabisa kwa sababu ni jambo la kawaida kutokea katika soka popote pale duniani, ” Aliongeza Vieira.

Magazeti ya Tanzania leo Machi 14, 2017
Gerard Pique: Wachezaji Wa Barca Sio Maroboti