Kiungo na Nahodha wa zamani wa Arsenal Patrick Vieira amesaini mkataba wa miaka mitatu na klabu ya Strasbourg inayoshiriki Ligi Kuu ya Ufaransa Ligue 1.
Vieira amesaini mkataba huyo ambao unamuwezesha kuwa Mkuu wa Benchi la Ufundi la Strasbourg, baada ya kuachana na Crystal Palace ya England ambayo alianza kuinoa tangu mwaka 2021 hadi mwaka huu.
Mkongwe huyo kutoka Ufaransa mwenye umri wa miaka 47, aliiongoza Palace kumaliza katika nafasi ya 12 na kufika Nusu Fainali ya Kombe la FA katika msimu wake wa kwanza akiwa kocha, lakini alitimuliwa katikati ya Machi baada ya kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Brighton & Hove Albion.
“Kuwasili kwa Patrick kunapaswa kuturuhusu kufanya maendeleo zaidi na kupiga hatua,” amesema Rais wa Strasbourg, Marc Keller.
“Analingana na wasifu tuliokuwa tunatafuta, Kocha mwenye uzoefu wa kimataifa, na ambaye ana ufahamu mzuri wa Ligue 1 na wachezaji wake wachanga.”
Klabu ya Strasbourg ilimaliza katika nafasi ya 15 katika msimu wa ligi wa 2022-23.
“Nina furaha hasa kujiunga na Racing,” amesema Vieira akiiambia tovuti ya klabu. “Ninajua historia na utambulisho wa klabu hii.”
Vieira alishinda Kombe la Dunia mwaka 1998 na Ubingwa wa Ulaya mwaka 2000 kama mchezaji wa Ufaransa. Aliichezea nchi yake zaidi ya mechi 100, akifunga mabao sita.
Katika ngazi ya klabu, aliisaidia Arsenal kushinda mataji matatu ya Ligi Kuu England na kushinda Serie A mara nne akiwa na AC Milan mwaka 1995 hadi 1996 na akiwa na Inter Milan katika misimu mitatu mfululizo kuanzia 2006-07.
Mfaransa huyo alianza maisha yake ya ukocha akiwa na timu yake ya zamani ya Manchester City chini ya umri wa miaka 23 kuanzia mwaka 2013 hadi 2015, kabla ya kuchukua mikoba ya New York City FC na kisha Klabu ya Nice ya Ligue 1.