Mlinda mlango kutoka nchini Hispania na klabu ya Espanyol Pau López Sabata, anakaribia kusajiliwa kwa mkopo na Tottenham Hotspurs yenye maskani yake makuu kaskazini mwa jijini London nchini England.

Spurs na Espanyol wamekua katika mazungumzo ya kina kuhusu uwezekano wa usajili wa mlinda mlango huyo mwenye umri wa miaka 21, ambaye tayari ameshaonyesha nia ya kujiunga na kikosi cha Mauricio Roberto Pochettino.

Pau anatarajiwa kuwa katika kikosi cha kwanza endapo atakidhi vigezo vya meneja wa Spurs, kufuatia mlinda mlango chaguo la kwanza wa klabu hiyo Hugo Lloris kupata majeraha katika mchezo wa ufunguzi wa ligi ya nchini England uliochezwa mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Everton.

Hata hivyo Pau jana alikua sehemu ya kikosi cha Espanyol kilichokua kikifanya maandalizi ya mwisho kabla ya kuanza kwa msimu wa ligi ya nchini Hispania mwishoni mwa juma hili, ambapo wakongwe hao wa Catalunha watapambana na Sevilla.

Taarifa ambazo zimeripotiwa mapema hii leo zimeeleza kuwa, mlinda mlango huyo huenda hii leo akaelekea jijini London tayari kwa kufanyiwa vipimo vya afya.

Pia imeelezwa kuwa, huenda akawa sehemu ya kikosi cha Spurs ambacho kitacheza mchezo wa mzunguuko wa pili wa ligi ya nchini England dhidi ya Crystal Palace hapo kesho.

 

David Moyes Ashtuka, Amrejesha Kundini Lamine Kone
Pep Guardiola Hajaridhishwa Na Usajili Alioufanya