Kikosi cha mabingwa wa soka barani Afrika mwaka 2017, jana jioni kilikaribishwa ikulu na rais Paul Biya, kwa ajili ya kupongezwa, kufuatia mafanikio waliyoyachuma nchini Gabon mwishoni mwa juma lililopita, kwa kuifunga Misri mabao mawili kwa moja.

Rais Biya aliwaalika wachezaji wa The Indomitable Lions, baada ya kuwasili mjini Yaunde siku ya jumatano na kulakiwa na wadau wa soka mjini humo.

Kabla ya kufika ikulu ya Cameroon, wachezaji wa timu hiyo walipita katika baadhi ya mitaa ya mjini Yaunde wakiwa katika gari la wazi, ikiwa ni sehemu ya kuendeza shangwe na furaha mbele ya mashabiki wa soka nchini humo.

Mbali na kuvishwa medali za dhahabu wakiwa mjini Libreville kama mabingwa wa Afrika mwaka 2017, Rais Biya jana aliwavisha nishani za heshima wachezaji wote wa timu ya taifa lake, na aliwataka kuendelea kuwa na moyo wa kizalendo.

Baada ya hafla ya kuwapongeza wachezaji, rais Biya alipiganao picha ya pamoja, kwa ajili ya kumbukumbu akiwa sambamba na mkewe (First Lady) Chantal Biya.

Kama hiyo haitoshi mke wa rais wa Cameroon alipiga hatua nyingine zaidi kwa kumuomba mlinda mlango bora wa kikosi cha The Indomitable Fabrice Ondoa kupiga nae ‘selfie’.

Mafanikio ya kutwaa ubingwa wa Afrika, yamemaliza ukame uliodumu katika kikosi cha Cameroon kwa kipindi cha miaka 15 iliyiopita, ambapo kwa mara ya mwisho walitwaa ubingwa wa AFCON mwaka 2002.

Cameroon watakua wenyeji wa fainali zijazo za AFCON mwaka 2019, na hatua hiyo inachukuliwa kama changamoto kwao ya kuhakikisha wanatetea ubingwa katika ardhi ya nyumbani.

NEC yahimiza vyama vya siasa kutoa elimu ya mpiga kura
Copa del Rey: Ni Alaves Na FC Barcelona