Meneja wa FC Barcelona Xavi amesitisha mpango wa kumsajili Kiungo kutoka nchini Ufaransa na klabu ya Manchester United Paul Pogba, baada ya kujiridhisha mchezaji huyo anakosa wasifu wa klabu hiyo.
Mkataba wa Pogba na Manchester United unamalizika mwishoni mwa msimu huu, na amekuwa akihusishwa na baadhi ya klabu vigogo Barani Ulaya, ambao ni PSG na FC Barcelona.
Tayari Xavi ameshakutana na Rais wa FC Barcelona Joan Laporta na kumtaka abadilishe mpango wa kumsajili Pogba, badala yake aelekeze nguvu hizo kwa mchezaji mwingine.
Taarifa za awali zinasema wakala wa Pogba, Mino Raiola, alikutana na Rais wa klabu Joan Laporta nchini Italia mwanzoni mwa Juma hili ili kujadili uwezekano wa usajili wa wateja wake wanne, watatu kati yao wakikata kandarasi msimu ujao wa joto.
Pogba, Xavi Simons wa PSG na Noussair Mazraoui wa Ajax wote mikataba yao inaisha msimu wa joto huku mteja wa nne wa Raiola, Erling Haaland, ataweza kuhama kwa bei pungufu mara tu ya msimu utakapomalizika.
Haaland atakuwa sokoni kwa dau la pauni milioni 64 kutokana na kifungu cha mkataba wake na bado ni kipaumbele cha wababe hao wa Catalan.