Kiungo wa Juventus, Paul Pogba amekiri kwamba alifikiria kustaafu soka kufuatia madai ya unyang’anyi yaliyohusisha familia.
Kiungo huyo wa kimatafa wa Ufaransa alitishwa na genge la watu wasiojulikana ambao walifunika nyuso ikidaiwa walimfosi kutoa mamilioni ya pesa huku kaka yake Mathias Pogba akihusishwa katika mpango huo wa kiharamia.
Mathias alichunguzwa na polisi kutokana na madai hayo aliyohusishwa akiwa mahabusu pamoja na watu wengine wanne kwa miezi miezi mitatu mwaka jana.
Kaka huyo wa Pogba alikana shutuma hizo akidai hana hatia katika jaribio la unyang’nyi dhidi ya ndugu yake na aliachiwa huru kufuatia amri ya mahakama na alipigwa marufuku kuwasiliana na mdogo wake.
Kiungo huyo aliyewahi kubeba Kombe la Dunia 2018 aliripoti polisi kutoa ushahidi na amezungumzia sakata hilo lilivyoiathiri familia yake.
“Pesa zinabadili tabia ya mtu. Familia inaweza kuvunjika. Vita inaweza kutengenezwa,” alisema Pogba.
“Kuna wakati nilikuwa nikifikiria nilitamani kutokuwa na pesa tena. Sikutaka kucheza soka tena, nilitaka nibaki kuwa mtu wa kawaida watu wanipende kama mimi na sio kwa sababu ya umaarufu wangu. Kuna wakati inakuwa ngumu sana.”
Pogba aliwaambia polisi kwamba genge hilo la wahuni lilianza kumtishia tangu Machi, mwaka jana huku likimsisitiza atoe Pauni ll milioni.
Baada ya kuvamiwa na genge hilo lililokuwa na silaha, Pogba alilazimika kutoa Euro 100,000 ili kulituliza lakini liliendelea kumsumbua.
Inasemekana kiungo huyo alisumbuliwa na vitisho tangu alipokuwa Manchester United kabla ya kuondoka na baada ya kujiunga na Juventus.