Shirikisho la soka nchini Kenya (FKF) limeanza mchakato wa kumsaka kocha mpya wa kikosi cha Harambee Stars, baada ya kocha Paul Put kujiuzulu ikiwa ni miezi mitatu tu, tangu alipokabidhiwa majukumu ya kuwa mkuu wa benchi la ufundi la timu ya taifa ya nchi hiyo.
Hii ilithibitishwa jana Jumatatu, na shirikisho la soka nchini humo FKF kupitia meneja wa mawasiliano na uhusiano Mwema Barry Otieno ambaye alielezea kuwa kocha huyo alijiuzulu kutokana na matatizo binafsi huku Stanley Okumbi akichukua nafasi yake kwa muda.
”Shirikisho la soka la Kenya lingependa kuwaambia mashabiki wa soka nchini Kenya kwamba bwana Pual Put amejiuzulu rasmi kama mkufunzi wa timu ya taifa kutokana na maswala ya kibinafsi.
”Hatahivyo kujiuzulu kwa kocha huyo ni pigo katika harakati za timu ya taifa kuelekea katika kufuzu mashindano ya AFCON 2019 kwa kuwa alikuwa kiungo muhimu cha timu”.
Na kufuatia hatua hiyo FKF imeanza mchakato wa kutafuta suluhu ya kujaza wadhfa wa Put huku Stanley Okumbi akichukua mahala pake kwa muda.
”Mwisho FKF inamshukuru bwana Put kwa huduma zake wakati akiwa mkufunzi mkuu wa Harambee Stars mbali na kumtakia mema katika kazi yake siku zijazo”, taarifa hiyo ilisema.