Kiungo wa zamani wa Manchester United, Paul Scholes amemwambia winga Antony kile anachopaswa kufanya ili kuepuka kukosolewa na wachambuzi wa soka.
Antony, ambaye amevumilia kipindi kigumu akiwa na Mashetani Wekundu msimu huu, aliwakashifu wachezaji wa zamani wa Man United, akisema kwamba ukosoaji wao hauwajengi bali unawavuruga zaidi.
Winga huyo aliyesajiliwa kwa Pauni 85 milioni hajafunga au kutoa pasi ya bao katika mashindano yote aliyocheza msimu huu, licha ya kucheza mechi 14.
Mbrazili huyo ameandamwa na wachezaji wa zamani wa Man United wakikosoa kiwango chake, akiwamno mshambuliaji wa zamani klabu hiyo Dimitar Berbatov na beki Gary Neville.
Scholes amempa ushauri nyota huyo wa zamani wa Ajax alipokuwa akijibu hoja ya Antony, akiandika kupitia akaunti yake ya Instagram: “Kimbia kwa kasi juu na chini, funga mabao, na utengeneze malengo yako pia.”
Winga huyo alishtakiwa kwa kosa la kumpiga mpenzi wake wa zamani Gabriela Cavallini, hata hivyo alikana shutuma hizo na kesi hiyo imekuwa kimya kwa sasa.
Antony alianza katika mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Chelsea Jumatano usiku, na alionyesha kiwango kizuri, huku Man United ikiibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Chelsea.
Mabao ya Man United yaliwekwa kimiani na kiungo Scott McTominay dakika ya 19 na 69, huku bao Chelsea likifungwa katika dakika ya 45 na kinda Cole Palmer, ambaye amezifunga karibu klabu kubwa zote alizokabiliana nazo.