Bao lililofungwa na mshambuliaji kutoka nchini Argentina Paulo Bruno Exequiel Dybala kwa njia ya mkwaju wa penati, lilitosha kuwavusha mabingwa wa soka nchini Italia Juventus FC katika hatua ya 16 bora ya ligi mabingwa barani Ulaya dhidi ya FC Porto ya Ureno.
Dybala alifungwa mkwaju huo wa penati, baada ya mwamuzi kutoka nchini Romania Ovidiu Hațegan kujiridhisha beki wa FC Porto Maximiliano Pereira, aliushika kwa makusudi mpira uliokua unaelekea langoni.
Beki huyo pia alionyeshwa kadi nyekundu kwa kosa hilo.
Juventus wamesonga mbele kwa jumla ya mabao matatu kwa sifuri, ambapo inakumgbukwa katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliounguruma mjini Porto nchini Ureno waliibuka na ushindi wa mabao mawili kwa sifuri.
Michuano hiyo inaendelea tena hii leo kwa michezo mingine miwili ya hatua ya 16 bora ambapo Atletico Madrid watakuwa nyumbani Vicente Calderón Stadium wakiwakabili Bayer Leverkusen kutoka nchini Ujerumani, ambao katika mchezo wa kwanza walikubali kufungwa mabao manne kwa moja.
Mjini Monaco nchini Ufaransa napo kutapigwa mchezo mwingine wa michuano hiyo kati ya AS Monaco dhidi ya Man City kutoka England.
Wawili hao walipokutana mjini Manchester majuma mawili yaliyopita, ilishuhudiwa Man City wakiibuka na ushindi wa mabao matano kwa matatu.