Nahodha na beki wa zamani wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Boniface Pawasa ametoa somo kwa mabeki wa klabu za Ligi Kuu, ili kufaulu mtihani wa kumkaba mshambuliaji wa pembeni wa Young Africans Tuisila Kisinda ‘TK Master’.

Pawasa ametoa somo hilo, kufuatia uwezo wa Kisinda kuenekana mtihani kwa mabeki wa klabu za Ligi Kuu, ambao kwa asilimia kubwa wameshindwa kutambua namna ya kumzuia.

Pasawa amesema amemfuatilia kwa ukaribu winga huyo kutoka DR Congo na amebaini mapungufu yake, ambayo kwa kiasi kiubwa yameshindwa kubainika kwa urahisi na mabeki aliowahi kukutana nao tangu alipoanza kuitumikia Young Africans mwanzoni mwa msimu huu.

“Tuisila hatakiwi kupewa nafasi, beki namba mbili na beki wa kati ndio wanapaswa kuwasiliana namna ya kumkabili, ndipo wanaweza wakapunguza makali yake, kwani si mchezaji ambaye anaingia ndani ya eneo la penalti, huwa anakimbilia pembeni hiyo ndio nafuu yao, lasivyo angekuwa anawaliza mara kwa mara,” amesema Pawasa ambaye kwa sasa ni kocha wa timu ya taifa ya soka la ufukweni.

“Tuisila hafikii mbio alizokuwa nazo Said Maulid ‘SMG’ wakati wa kumkaba, tukiona mpira umepigwa kwake, mmoja anabaki nyuma, mwingine anaenda kukabana naye bila kumwachia nafasi, mbaya zaidi alikuwa anamlazimisha beki amfanyie makosa ndani ya eneo la penalti, ndio maana jina lake lina nguvu hadi leo, kitu ambacho Tuisila anakikosa.”

“Laiti Tuisila angekuwa ananyanyua macho yake kuona anaenda wapi angekuwa hatari zaidi, pia awe anaangukia ndani ya eneo la penalti na sio anavyofanya kutumia nguvu nyingi, wakati mwingine haziifaidishi timu, ila ni mchezaji mzuri sana anayetakiwa kuonge-zewa maarifa kidogo sana,” amesema.

‘TK Master’ alijiunga na Young Africans akitokea AS Vita ya kwao DR Congo na mpaka sasa amekua msaada mkubwa ndani ya kikosi cha Wananchi ambacho kinaongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, huku kikitwaa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi.

Azam FC kumaliza na Kombaini ya Zanzibar
CHAN 2021: Taifa Stars shughulini leo

Comments

comments