Meneja wa Klabu ya Manchester City, Pep Guardiola amesifia uwezo na mwenendo wa beki John Stones ambaye alimsajili mwanzoni mwa msimu huu akitokea Everton.
Guardiola alikubali kutoa kitita cha Pauni milioni 47.5 kwa ajili ya usajili wa beki huyo, ambaye alizusha tafrani kwenye baadhi ya vyombo vya habari, ambavyo vilidai hakustahili gharama hiyo.
Wachambuzi mbalimbali kupitia vyombo vya habari walieleza kuwa waliamini uwezo wa Stones ni wa kawaida na alipaswa kusajiliwa kwa kiasi cha pesa ambacho kingeendana na uwezo wake anapokua uwanjani.
Kwa mara ya kwanza Guardiola amewajibu waandishi wa vyombo vya habari kwa kusema, anajivunia kuwa na Stones tangu mwanzoni mwa msimu huu, na ameonyesha uwezo mkubwa wa kuiboresha safu yake ya ulinzi.
Guardiola alitoa sifa kwa beki huyo kutoka nchini England, alipozungumza na waandishi wa habari mara baada ya mchezo wa jana, ambapo Man city walilazimisha sare ya bao moja kwa moja dhidi ya Liverpool katika ligi ya England.
“Stones alipatwa na maswahibu mengi ya kupingwa na vyombo vya habari, kwa kigezo cha pesa iliyotumika kumsajili, lakini hii leo (Jana) ameonyesha uwezo mkubwa ambao utakua umesaidia kujibu tuhuma alizokua akirushiwa na baadhi ya vyombo vya habari,” Alisema Guardiola.
“Nimekua mtetezi wake kwa kipindi kirefu, ila acha niseme hadharani kwa kueleza kuwa, Stones ni mchezaji mwenye viwango vyote vya kucheza hapa, na alistahili kusajiliwa na kiasi cha pesa kilichotumika kumng’oa Everton.”