Matajiri wa mjini Manchester (Man City) wamekubali kumsajili beki wa kulia wa Tottenham Hotspur Kyle Walker kwa kiasi cha Pauni milioni 50.
Walker alikua akihusishwa na mipango ya kutaka kusajiliwa na matajiri hao tangu kipindi hiki cha usajili wa majira ya kiangazi kilipoanza, hali ambayo imemnyima nafasi ya kusafiri na kikosi cha Spurs, ambacho kwa sasa kipo nje ya England kikijiandaa na msimu mpya wa ligi.
Man city wamekubali kumsajili beki huyo, baada ya kushindwa kukamilisha mpango wa kumnasa beki wa kulia kutoka nchini Brazil Dani Alves ambaye jana alitambulishwa rasmi na uongozi wa PSG.
Man City wamekua na hitaji la beki wa pembeni baada ya kuwaruhusu Gael Clichy, Pablo Zabaleta na Bacary Sagna kuondoka mwishoni mwa msimu uliopita, na wameanza na Walker katika harakati za kuziba nafasi hizo.
Pia wanatajwa kuwa katika mipango ya kumsajili beki wa pembeni wa mabingwa wa soka nchini Ufaransa AS Monaco Benjamin Mendy.