Klabu ya Manchester City imeshinda taji lao la tano la Ligi Kuu ya England ndani ya misimu sita baada ya Arsenal kufungwa 1-0 na Nottingham Forest Jumamosi (Mei 20), huku Meneja Pep Guardiola akisema mashabiki wao ndio chachu kubwa.
Kufungwa kwa Washika bunduki hao walionyuma ya Man City kwa pointi saba kwenye msimamo wa Ligi huku wakiwa wamebakiwa na mchezo mmoja pekee kuchezwa, kulimaanisha kuwazawadia taji hilo kabla ya mchezo wa jana Jumapili (Mei 21) dhidi ya Chelsea iliyokubali kulala 1-0.
Vijana wa Guardiola walitumia muda mwingi wa msimu huu kuwawinda Arsenal, na walipata nafasi nzuri zaidi bada ya ushindi wao wa 4-1 kule Etihad mwezi uliopita.
Nyota wa Norway, Erling Haaland, ambaye alivunja rekodi ya mabao kwenye ligi hiyo, aliwafanya City kuwa kileleni, huku pia wakiwania kutwaa mataji mengine mawili msimu huu (FA na Ligi ya Mabingwa Ulaya) ambapo yote wametinga fainali.
Guardiola amezungumzia kuungwa mkono na mashabiki wao kuwa moja ya sababu ya kuamua ushindi wao msimu huu.
Amesema: “Mashabiki wetu wa ajabu wamekuwa nasi kila hatua kwenye safari hii. Bila msaada wao wa ajabu sidhani kama kuna njia yoyote ambayo tungeweza kufikia kile tumefanya misimu sita iliyopita.”
“Shauku na uungwaji mkono wao imekuwa muhimu sana na ya kutia moyo kwetu sote. Tunatumaini kushinda taji la Ligi Kuu tena ni njia muafaka kwetu kusema asante kwa mashabiki wetu.”
Naye Nahodha na Kiungo wa Man City, Ilkay Gundogan alikuwa mtu muhimu sana wakati wa kinyang’anyiro cha timu yake na aliipongeza timu nzima nyuma ya kunyakua taji la tatu mfululizo.
Amesema: “Kuisaidia Klabu kushinda taji la tatu mfululizo la Ligi Kuu ni jambo la kipekee sana.
“Ligi Kuu England bila shaka ndiyo yenye ushindani mkubwa duniani hivyo inakuambia kila kitu kuhusu mafanikio haya.
“Pia ningependa kumshukuru Pep, wafanyakazi wote na kila mtu anayefanya kazi katika klabu hii ya soka.
“Kila siku wanasaidia kutupatia wachezaji kila kitu tunachohitaji ili kujaribu kupata mafanikio.
“Kushinda kombe hili mara tatu mfululizo na mara tano katika miaka sita ni jambo la kushangaza. Ubora huo na uthabiti husaidia kuhitimisha kile ambacho Manchester City inasimamia na kuhakikisha Klabu itaendelea kujitahidi kupata mafanikio ya kusonga mbele.
“Umekuwa msimu ambao sitausahau kamwe.”