Kocha Mkuu wa Manchester City, Pep Guardiola, amebainisha kwamba, kitendo cha kubeba mataji matatu msimu uliopita 2022/23, kimezidi kuwapa nguvu ya mapambano msimu huu 2023/24, ambapo anataka kuweka rekodi mpya.
Guardiola msimu uliopita aliiongoza Man City kushinda mataji matatu ambayo ni Ligi Kuu ya England, Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya na Kombe la FA.
Kocha huyo ambaye ana takribani miaka saba klabuni hapo, msimu huu anasaka rekodi ya kubeba taji la Ligi Kuu England kwa mara ya nne mfululizo.
“Kushinda mataji matatu kumetupa nguvu kubwa sana, msimu huu tunataka kuendelea kuwa bora.
“Nimekuwa nikisema mara kwa mara kwamba, hakuna aliyeshinda mataji manne mfululizo ya Premier, hakuna, hivyo unaona ni namna gani hali ilivyokuwa ngumu.
“Kipindi hiki, tuna mechi nyingi muhimu, tukianzia UEFA, tutacheza mara mbili na Young Boys, baada ya hapo, akili zote tutazihamishia Premier, ni muhimu kuendelea kufanya vizuri,” amesema Guardiola.
Kocha huyo ameshinda mataji matano ya Premier akiwa na Man City. Amechukua mara mbili mfululizo 2017/18 na 2018/19, kisha mara tatu mfululizo 2020/21, 2021/22 na 2022/23.