Matajiri wa jiji la Manchester Man City wameonyesha dhamira ya kutaka kumsajili beki wa pembeni kutoka nchini Brazil na klabu bingwa nchini Italia Juventus FC, Dani Alves.
Meneja wa Man City Pep Guardiola anaamini beki huyo atakubali kujiunga na Man City mwishoni mwa msimu huu, kufuatia ukaribu uliopo kati yake na Alves, ambaye alifanyanae kazi katika klabu ya Barcelona.
Alves alisajiliwa na Guardiola mwaka 2008 na kujiunga FC Barcelona akitokea Sevilla CF, na alifanikiwa kuwa sehemu ya kikosi cha kwanza cha meneja huyo ambaye alipata mafanikio makubwa katika kipindi kifupi.
Licha ya umri mkubwa wa beki huyo ambaye kwa sasa ana miaka 33, bado imeripotiwa kuwa Guardiola anaamini Alves ana uwezo mkubwa wa kucheza soka, na kama atafanikiwa kumpeleka Man City atakua amekata kiu ya kuhitaji beki wa upande wa kulia.
Kwa sasa Man City inawategemea Pablo Zabaleta na Bacary Sagna kama mabeki wa upande wa kulia, lakini Guardiola ameona kuna umuhimu wa kumsajili Alves, ili kuleta changamoto kwa wawili hao.