Meneja wa Mabingwa wa Soka nchini England Manchester City Pep Guardiola amesisitiza michezo mitatu ijayo ndiyo itakayoamua mbio za ubingwa baada ya ushindi wa mabao 4-1 walioupata dhidi ya Arsenal katika mchezo wa Ligi Kuu England juzi Jumatano (Aprili 26).
City wamebakia katika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi hiyo wakiwa alama mbili nyuma vinara Arsenal lakini wakiwa na mchezo mmoja mkononi dhidi ya wapinzani wao, huku ikibakiza michezo saba pekee msimu kumalizika.
Mabao mawili kutoka kwa Kevin De Bruyne, John Stones na Erling Haaland wakifunga moja kila mmoja yaliimarisha kiwango chao nyumbani, lakini Guardiola alikuwa mwepesi kuelekeza macho katika mechi muhimu zilizokuwa mbele yao.
“Najua michezo mitatu ijayo ni muhimu sana,” alisema akizungumza na BT Sport.
“Fulham (itakayochezwa Jumapili), alichofanya Marco Silva msimu huu ni cha kushangaza, na kisha baada ya mechi mbili za nyumbani dhidi ya West Ham na Leeds, michezo hii itaamua msimu.”
“Ukweli leo (juzi), tuko nyuma ya Arsenal, wako pointi mbili mbele yetu.” Guardiola aliendelea kusifu njia kuu ya ushindi wa timu yake ambayo sasa imeshinda michezo 12 mfululizo ya ligi dhidi ya Arsenal.”
“Kuanzia dakika ya kwanza tulikuwa na umakini mkubwa,” Guardiola alisema.
“Sisi ni washindi mfululizo wa ligi, ukipoteza mchezo unasema una muda lakini Arsenal haikuwa hivyo. Wachezaji wanajua ni karibu na kama tunapoteza, hatuna nafasi.”