Beki kutoka nchini Ujerumani Per Mertesacker amewahimiza wachezaji wenzake wa klabu ya Arsenal, kupambana ili kufikia lengo la kucheza fainali ya Europa League na kutwaa ubingwa wa michuano hiyo.
Mertesacker amehimiza jambo hilo, kwa kutaka kutoa heshima kwa meneja wao Arsene Wenger ambaye mwishoni mwa juma lililopita alitangaza kuondoka klabuni hapo, baada ya kudumu kwa miaka 22.
Mertesacker amesema litakua jambo la heshima kwa meneja huyo kutoka nchini Ufaransa, ambalo litafanywa na wachezaji wake ambao wamebahatika kufundishwa babu huyo katika zama zake ya mwisho klabuni hapo.
Amesema mzee huyo hajawahi kutwaa ubingwa wowote wa barani Ulaya, hivyo ni wakati mzuri wa kuhakikisha heshima yake inatunzwa kwa vitendo, kupitia michuano hiyo ambayo keshokutwa watacheza hatua ya nusu fainali dhidi ya Atletico Madrid.
“Tunapaswa kuwajibika ipasavyo ili kumzwadia heshima Arsene Wenger, tutakua tumempa zawadi ambayo hatoisahau katika maisha yake tangu alipoanza kufundisha soka klabuni hapa, endapo tutafanikiwa kutwaa ubingwa wa Europa League,” Amesema Mertesacker
“Timu yote kwa ujumla inapaswa kutambua umuhimu wa jambo hili, hata ikitokea siku za usoni tunafikia lengo la kufika mbali katika michuano hii, lakini haitokua kama wakati huu ambao tunapaswa kuweka heshima kwa bosi wetu.”
Mpaka Arsene Wenger anatangaza kuondoka klabuni hapo, tayari ameshafanikiwa kutwaa ubingwa wa England mara tatu na kombe la chama cha soka nchini humo FA mara saba.
Endapo Arsenal watachukua ubingwa wa Europa League haitokua heshima kwa Arsene Wenger pekee, bali kwa upande wa klabu kwa ujumla kwani hawajawahi kushindwa taji hilo.