Watafiti kutoka nchini Marekani wamesema kuwa wamekamilisha majaribio yaliyofanikiwa kwa wasichana nchini humo ya pete inayowekwa sehemu za siri za mwanamke kwa lengo la kuzuia maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU).
Kwa mujibu wa shirika la habari la BBC, watafiti hao ambao ni jopo la wataalam wa masuala ya afya wamesema kuwa zoezi hilo linahamia kwa mabinti barani Afrika.
Zoezi hilo hufanywa kwa kuweka pete ya plastiki ukeni, pete ambayo huwekewa dawa za kupunguza makali ya virusi vya ukimwi, kwa lugha ya kiingereza Anti-Retroviral (ARV) na hubadilishwa mara moja kwa mwezi.
Wataalam hao wanadai kuwa utafiti uliofanywa kwa mabinti wa Marekani kwa muda wa miezi sita ulionesha mafanikio makubwa.
Wakieleza matokeo ya utafiti huo katika mkutano kuhusu sayansi na Virusi vya Ukimwi uliofanyika hivi karibuni jijini Paris nchini Ufaransa, watafiti hao wameeleza kuwa wamepata nguvu zaidi baada ya wasichana waliofanyiwa majaribio kusema kuwa wamezipenda pete hizo za plastiki.
Utafiti huo unatokana na utafutaji wa njia ya wanawake kuweza kujilinda dhidi ya virusi vya ukimwi wakati wa kujamiiana bila kutegemea wanaume kuvaa mipira (condoms).
Ripoti inaonesha kuwa asilimia hamsini ya maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi yako kwa wasichana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24 na kwamba takribani jumla ya vijana na mabinti 1,000 huambukizwa virusi vya ukimwi katika ukanda wa Jangwa la Sahara.