Mchezaji wa Simba SC Peter Banda amesema haikuwa kazi rahisi kupata tuzo ya mchezaji bora wa mashabiki wa mwezi Machi kutokana uwezo mkubwa wa wachezaji ambao ameingia nao kwenye kinyang’anyiro.

Banda ameyasema hayo wakati alikabidhiwa tuzo ya mchezaji bora wa mwezi Machi wa wadhamini Emirate Aluminium ACP katika ofisi zao zilizopo Sinza Madukani.

Banda amesema Simba ina wachezaji bora wengi na ushindani ni mkubwa na kuanzishwa kwa tuzo hizi zinaongeza chachu ya ushindani.

Banda amelishukuru benchi la ufundi, wachezaji na mashabiki waliompigia kura na kusababisha kupata tuzo hiyo kwake ni kitu kikubwa.

“Haikuwa kazi rahisi kupata tuzo hii Simba ina wachezaji wazuri wengi. Naushukuru benchi la ufundi na wachezaji kwa ushirikiano walionipa. Pia nawashukuru mashabiki kwa kunipigia kura nyingi, naamini nitaendelea kufanya vizuri,” amesema Banda.

Kwa upande wake Ofisa Habari na Mawasiliano wa Emirate Aluminium ACP, Issa Maeda amesema kampuni yao inaendelea kutangazwa kimataifa kwakuwa mashabiki wengi kutoka nje wanawapigia kura wachezaji wao.

“Ukiangalia takwimu Banda amepigiwa kura na mashabiki wengi kutoka nyumbani kwao Malawi, iliwahi kutokea kwa Joash Onyango Wakenya walipiga kura sana pia Clatous Chama naye Wazambia wengi walimpigia kura hivyo Emirate inazidi kutangazika,” amesema Maeda.

Banda amekabidhiwa tuzo pamoja na pesa taslimu Sh. 2,000,000 kutoka kwa Emirate Aluminium ACP. Katika mwezi Machi amecheza dakika 226 ndani ya Mechi nne na kutoa assist moja.

Dkt.Biteko:Madini yaongeze amani ukanda wa Maziwa Makuu
Tshabalala awashukuru Mashabiki Simba SC