Mlinda mlango wa zamani wa timu ya taifa ya Denmark Peter Schmeichel amesema beki wa pembeni wa England, Kyle Walker alipaswa kuadhibiwa kwa kadi nyekundu kufuatia tukio la kumpiga kiwiko Fakhreddine Ben Youssef wa Tunisia, wakati wa mchezo wa kundi G uliochezwa usiku wa kuamkia leo.
Beki huyo wa klabu ya Man City alifanya kitendo hicho dakika ya 35 na kusababisha mkwaju wa penati kupigwa langoni mwa England, na kuifanya timu taifa ya Tunisia kupata bao la kusawazisha.
Schmeichel ambaye aliwahi kutamba na klabu za Man City, Man Utd na Aston Villa, amesema kutokana na uzito wa kosa lililofanywa na Walker, mwamuzi hakupaswa kumuonyesha kadi ya njano, kwani alifanya tukio hilo kwa kukusudia baada ya kuona hana uwezo wa kuufikia mpira uliokua umepigwa kutoka upande wa kulia wa lango la England.
“Ilikua penati dhahir, Walker alimpiga kiwiko Fakhreddine Ben Youssef kwa makusudi, na haikupaswa kupewa kadi ya njano, ukiangalia vizuri utaona namna alivyofanya tukio hilo kwa makusudi, hivyo kadi nyekundu ilikua inamuhusu.”
“Ilikua kama bahati kwake kuonyeshwa kadi ya njano, lakini kama mwamuzi angejiridhisha kwa kuangalia kwa mara ya pili kupitia VAR, Walker alikua anaadhibiwa maradufu.” Amesema Peter Schmeichel alipohojiwa na kituo cha Russia Today.
Katika mchezo huo, England walichomoza na ushindi, kufuatia bao lililofungwa dakika za lala salama na mshambuliaji na nahodha wao Harry Kane ambaye jana alikua msaada mkubwa kwa timu hiyo.
England walitangulia kufunga bao dakika ya 11 kupitia kwa Harry Kane kabla ya Tunisia hawajasawazisha kwa mkwaju wa penati uliopigwa na Ferjani Sassi dakika ya 35.