Mlinda mlango wa kikosi cha Arsenal Petr Cech huenda akawa nje ya uwanja kwa majuma manne, baada ya kuumia kiazi cha mguu akiwa katika mchezo wa ligi ya England mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya West Brom.
Mlinda mlango huyo kutoka Jamuhuri ya Czech jana alifanyiwa vipimo na imebainika jeraha lake litahitaji karibu mwezi mmoja, ili kupona vizuri.
Matarajio ya kukaa nje kwa mlinda mlango huyo, yanamaanisha ataikosa baadhi ya michezo ya ligi ambayo itaikabili Arsenal, ukiwepo mpambano dhidi ya Man City ambao unatarajiwa kuunguruma mwishoni mwa juma lijalo mjini London.
Cech, pia yupo katika hati hati ya kukosa mchezo wa nusu fainali ya kombe la FA, ambapa utawakutanisha na Man city kwenye uwanja wa Wimbley April 23.
Kuumiwa kwa Cech, kutatoa nafasi kwa mlinda mlango kutoka nchini Colombia David Ospina kuendelea kukaa langoni, baada ya kutumika kama mchezaji wa akiba mwishoni mwa juma lililopita ambapo Arsenal walikubali kichapo cha mabao matatu kwa moja kutoka kwa West Brom.
Ospina ataendelea kucheza mfululizo katika kipindi hiki, baada ya kuitwa katika timu yake ya taifa ya Colombia, hali ambayo hueneda ikamsaidia kuwa katika kiwango bora atakaporejea jijini London kwa ajili ya kuendelea na jukumu la kusimama langoni mwa Arsenal.