Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji – EWURA, inatangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta ya Petroli hapa nchini zitakazotumika kuanzia Jumatano, Agosti 2, 2023 ambapo bei za rejareja za mafuta katika Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga na Mtwara zimeainishwa.

Kwa upande wa Dar es Salaam Petroli ni Shilingi 3,199 Dizeli Shilingi 2,935 na Mafuta ya Taa Shilingi 2,668 ambapo Mkoa wa Tanga Bei ni Shilingi 3,271 Dizeli Shilingi 2,981huku Mafuta ya Taa yakiwa ni Shilingi 2,740 huku Mkoa wa Mtwara Petroli ikiwa ni Shilingi 3,271 Dizeli Shilingi 3,008 na Mafuta ya Taa Shilingi 2,714.

Mabadiliko ya bei za mafuta kwa mwezi Agosti 2023 yanatokana na changamoto za upatikanaji wa Dola za Marekani, mabadiliko ya sera za kikodi, kushuka kwa thamani ya Shilingi dhidi ya Dola ya Marekani, ongezeko la gharama za mafuta katika soko la dunia na gharama za uagizaji wa mafuta.

Aidha, Wafanyabiashara wa bidhaa za mafuta kwa rejareja wanatakiwa kuuza mafuta kwa bei zinazooneshwa kna hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wote watakaokiuka agizo hilo, huku EWURA ikiwakumbusha Wafanyabiashara wa bidhaa za mafuta kwa jumla na rejareja pamoja na jamii kuzingatia bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli kwa eneo husika.

Kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya mwaka 2015, kifungu namba 166, bei za bidhaa za mafuta ya Petroli zitaendelea kupangwa na soko na EWURA itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta.

Hata hivyo, Kampuni za mafuta ziko huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani isipokuwa bei hizo zisizidi bei kikomo (Price cap) au kuwa chini ya bei iliyoruhusiwa (Floor Price) kama zilivyokokotolewa kwa mujibu wa Kanuni za EWURA za Kupanga Bei za Mafuta za Mwaka 2023 zilizotangazwa kupitia Gazeti la Serikali Na. 421 la tarehe 23 Juni 2023.

Aidha, Vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana yakionesha bei za mafuta, punguzo, vivutio vya kibiashara vinavyotolewa na kituo husika. Pale ambapo inawezekana kuchagua, wateja wanashauriwa kununua bidhaa za mafuta katika vituo vinavyouza mafuta kwa bei nafuu zaidi ili kushamirisha ushindani.

Chirwa aongeza mzuka Kagera Sugar
Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Agosti 2, 2023