Beki na nahodha wa klabu ya Everton, Phil Jagielka hii leo anatarajia kuwaongoza kwa mara ya kwanza wachezaji wa timu ya taifa ya England, katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Ulaya dhidi ya Lithuania.

Jagielka, atawaongoza wenzake katika mchezo wa hii leo, akichukua nafasi ya mshambuliaji wa Man Utd, Wayne Rooney pamoja na msaidizi wake Gary Cahill wa klabu ya Chelsea ambao tayari wamesharuhusiwa kuondoka kambini.

Kocha mkuu wa timu ya taifa ya England, Roy Hodgson amethibitisha kumpa nafasi hiyo Jagielka, na anaamini atafanikisha vyema kutokana na uelewa na uzoefu alioupata akiwa na klabu yake ya Everton.

Hodgson amesema Jagielka, amekua na mahusiano mazuri na wachezaji wenzake wanapokua kambini na hakutokua na shaka na maamuzi aliyoyachukua na kumtangaza kuwa nahodha wa kikosi chake hii leo, ambacho kitakaribishwa LFF Stadium huko nchini Lithuania.

Jagielka, mwenye umri wa miaka 33, hii leo atakuwa akicheza mchezo wake wa 38 akiwa na timu ya taifa ya England.

Kikosi cha England kinakwenda katika mchezo huo huku baadhi ya wachezaji wake muhimu wakiwa wamesharuhusiwa kuondoka kambini kama Wayne Rooney, Garry Cahill, Michael Carrick, James Milner pamoja na Joe Hart baada ya mchezo dhidi ya Estonia uliochezwa mwishoni mwa juma lililopita.

Endapo kikosi cha England, kitachomoza na ushidni hii leo, kitakuwa kimejiwekea rekodi ya kufuzu kwa uhakika kwenye fainali za mataifa ya Ulaya, kwa kushika nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa kundi E.

Prezzo Wa Kenya Ampa Sapoti Magufuli
Sergio Aguero Nje Mwezi Mmoja