Kiungo Philippe Coutinho atavaa jezi namba saba msimu wa 2018/19 akiwa na klabu yake FC Barcelona, na kuachana na jezi namba 14 ambayo amekua akiitumia tangu alipotua klabuni hapo mwezi Januari akitokea kwa majogoo wa jiji Loverpool.
Uongozi wa FC Barcelona umemtunuku jezi namba 7, kiungo huyo ili kukidhi haja ya ombi lake tangu alipotua klabuni hapo, lakini ilishindikana kuitumia kutokana na kuwa tayari ilikua imeshasajiliwa kwa jina la Arda Turan kwa msimu wa 2017/18.
Arda Turan aliihama Barcelona mwezi januari mwaka huu na kujiunga kwa mkopo na klabu ya İstanbul Başakşehir, hivyo ilikua ni vigumu kwa namba ya jezi aliyokua akiitumia kutumika mara mbili kwa msimu mmoja.
Coutinho amekua shabiki mkubwa wa jezi namba saba, na kwa mara ya mwisho alivaa jezi yenye namba hiyo akiwa na klabu ya Inter Milan ya Italia, kabla hajahamia Liverpool mwaka 2013.
Akiwa Anfield mshambuliaji huyo alishindwa kutimiza lengo la kuvaa jezi yenye namba hiyo, na badala yake alikabidhiwa jezi namba 10, kufuatia chaguo lake kutumiwa na aliyekua mshambuliaji wa Liverpool kwa wakati huo Luis Suarez.
Kutimiza lengo la kuvaa jezi namba saba akiwa na klabu ya Barcelona, kunamfanya Coutinho kujiunga na wachezaji waliowahi kuvaa jezi hiyo katika historia ya Barca kama Luis Figo, David Villa na Henrik Larsson.
Kiungo huyo wa kibrazil alisajiliwa na Barcelona mwezi Januari kwa ada ya Pauni milioni 145, na tayari ameshacheza michezo 22 na kufunga mabao 10.