Majogoo wa jiji Liverpool, huenda wakampoteza kiungo mshambuliaji kutoka nchini Brazil, Philippe Coutinho ambaye anawaniwa vikali na klabu za FC Barcelona pamoja na Paris Saint-Germain.

Klabu hizo mbili ambazo ni mabingwa wa nchini Hispania pamoja na Ufaransa, zimekua katika vita baridi ya kumsajili kiungo huyo mwenye umri wa miaka 23, kwa kipindi cha majuma kadhaa sasa.

Kwa nyakati tofauti viongozi wa klabu hizo, wamekua wakifanya mazungumzo na uongozi wa klabu ya Liverpool, ili kuona uwezekano wa kuipata saini ya Coutinho.

Hata hivyo mpaka sasa uongozi wa Liverpool, haujazungumza lolote kuhusu uwezekano wa kumuachia kiungo huyo ambaye kwa sasa yupo nchini Marekani sanjari na timu yake ya taifa ya Brazil, ambayo inashiriki michuano ya Copa America.

FC Barcelona, wameutumia mwanya wa kiungo huyo kuwa katika kikosi cha Brazil kwa kumshawishi mshambuliaji wao Neymar ili kumshurutishe Coutinho akubali kujiunga nae Nou Camp na kuikataa PSG.

Wakati hayo yakifanywa na FC Barcelona, PSG wameshatangaza dau la Pauni milioni 25 ambalo wanaamini litatosha kumuhamisha Coutinho Anfield hadi Parc De Princes.

Kuna uwezekano mkubwa wa kiungo huyo kuondoka jijini Loverpool, kutokana na hitaji la kutaka kucheza michuano mikubwa barani Ulaya ambapo kwa upande wa Liverpool hawatokuwa sehemu ya klabu ambazo zitashiriki ligi ya mabingwa barani Ulaya.

FC Barcelona pamoja na PSG ni klabu ambazo zimeshakata tiketi ya kucheza michuano hiyo kutokana na kumaliza vinara katika misimamo ya ligi za nchi ya Hispania na Ufaransa msimu wa 2015-16.

Jamie Vardy Kufanyiwa Vipimo Vya Afya
Rais Wa Simba SC Atuma Salamu Za Mwezi Mtukufu