Gwiji wa klabu ya AC Milan, Philippo Inzaghi anaamini Romelu Lukaku atapata mafanikio akiwa na AS Roma licha ya watu kumbeza tangu alipotua kwa mkopo akitokea Chelsea.
Lukaku amekuwa akipondwa hatapata mafanikio akiwa na timu hiyo inayonolewa na kocha wa Chelsea, Jose Mourinho, lakini Inzaghi amesisitiza nyota huyo aliyewahi kuichezea Manchester United, anaweza akashinda makombe akishirikiana vizuri na wachezaji wenzake kwenye kikosi kama Paulo Dybala.
“Nilidhani atabaki Inter Milan, mwishowe akaondoka, ujio wake AS Roma unaweza kuwa na maana kubwa sana kwenye mbio za ubingwa Serie A, Lukaku anaweza kuleta mchango akiungana na Dybala vizuri, wana uwezo wa kuleta kitu kwenye kikosi cha Jose Mourinho halafu tutaona mwisho itakuwaje. Watu wanaweza kufiriki Lukaku hakuchagua timu sahihi lakini sidhani.”
Kauli ya mkongwe huyo haikutofautiana sana na kauli ya nyota wa zamani wa Roma, Gaetano DAgostino ambaye alisisitiza Lukaku ataongeza nguvu katika kikosi cha AS Roma baada ya kukamilisha uhamisho wake.
AS Roma ilimsajili Lukaku kwa mkopo wa msimu mzima na italipa ada ya Pauni 8 milioni baada ya kukubaliana na Chelsea, ingawa kiungo huyo hana matumaini kama Lukaku ataweza kuisaidia AS Roma katika mbio za ubingwa msimu huu.
DAgostino alisema: “Ujio wake utaongeza nguvu katika kikosi, lakini sidhani kama atakuwa na mchango katika mbio za ubingwa. Nikiangalia maeneo mengine timu bado haijakamilika, safu ya ulinzi bado haina nguvu, Jose Mourinho anaweza kubadilisha mfumo.”