Mabingwa wa Soka nchini Ujerumani FC Bayern Munich na Klabu ya Liverpool zimeonyesha nia ya kutaka kumsajili kiungo wa Manchester City, Kalvin Phillips, kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili.
Phillips mwenye umri wa miaka 27 amekuwa hapati nafasi ya kutosha kwenye kikosi cha kwanza cha Man City tangu aliposajiliwa mwanzoni mwa msimu uliopita 2022/23 akitokea Leeds United.
Mapema kwenye dirisha hili aliweka wazi mpango wake ni kuendelea kusalia Man City na kupambania nafasi kwenye kikosi cha kwanza ingawa uwezekano unazidi kuwa mdogo siku hadi siku.
Munich inataka kumsajili staa huyu kutokana na msukumo mkubwa kutoka kwa kocha wao Thomas Tuchel anayedaiwa alihitaji huduma yake tangu alipokuwa anaifundisha Chelsea.
Liverpool yenyewe inamuhitaji Philips ili kuboresha eneo lao la kiungo na mara kadhaa ilijaribu kuwasajili Moises Caicedo na Romeo Lavia lakini wakazidiwa kete na Chelsea. Hadi sasa Phillips hajacheza hata mechi moja tangu kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu ya England.