Kocha wa Simba SC, Roberto Oliveira “Robertinho’ anaishi na hesabu zake akiamini timu yake imekamilika na sasa ameibuka na mkakati wa kiatu cha ufungaji bora.
Akizungumza jijini Dar es salaam, Robertinho amesema amefanya kikao na washambuliaji wake wawili, Jean Baleke na Moses Phiri kisha akawapangia malengo ya kufunga mabao ya kutosha msimu huu.
Robertinho amesema ameangalia mara ya mwisho Simba SC kuchukua ufungaji bora kwa mshambuliaji kabla kiungo wao mshambuliaji, Said Ntibazonkiza ‘Saido’ ilikuwa msimu wa 2020/21 na sasa anataka kuona wawili hao wanarudia anga hizo.
Msimu huo, Simba SC ilichukua kiatu cha ufungaji bora kilichokwenda kwa nahodha John Bocco, aliyefunga mabao 16, akifuatiwa na mwenzake, Chris Mugalu (mabao 15) wote wakiwa washambuliaji.
“Msimu uliopita Saido alionyesha uwezo mkubwa, lakini msimu huu nina malengo makubwa na Baleke na Phiri nadhani ni wakati muafaka kwa washambuliaji kurudi kwenye makali kama haya ya kufunga zaidi.
“Nimewaambia kila mmoja anatakiwa kuongeza umakini wa kutumia nafasi kwenye mechi zetu, kwa kuwa sasa tunatengeneza nafasi nyingi, Simba SC ni klabu kubwa inatakiwa kutawala kila kitu,” amesema Robertinho.
Robertinho ameongeza kikosi chao cha msimu huu kina viungo wa kutosha ambao wanajua kutengeneza nafasi za kufunga, huku wakiendelea kufurahia ubora mkubwa wa mabeki wawili wa pembeni.
“Tuna viungo bora sana wa katikati na pembeni, angalia Chama (Clatous), Saido, Onana (Willy), Luis (Miquissone), hawa wote ni vigumu wamalize dakika 90 bila kutengeneza nafasi za kufunga,” amesema.