Baada ya kurejea rasmi mazoezini kujiandaa na mchezo wao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Coastal Union, Kocha Mkuu wa Simba SC, Roberto Olivieira ‘Robertinho’ amewachimba mkwara mzito Washambuliaji wa timu hiyo, Moses Phiri na Jean Baleke kuhakikisha wanarekebisha makosa yao na kutumia vizuri kila nafasi wanazotengeneza.
Simba SC kwa sasa wanaendelea na kambi ya maandalizi ya michezo yao ijayo ambapo kesho (Septamba 21) Alhamisi watavaana na Coastal mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kabla ya kurudiana na Power Dynamos katika mchezo wa mkondo wa pili wa hatua ya pili ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Simba SC wataingia katika michezo hii wakiwa na kumbukumbu ya matokeo ya sare mabao 2-2 kwenye mchezo dhidi ya Dynamos uliopigwa Jumanmosi (Septemba 16) iliyopita.
Robertinho amesema: Ulikuwa mchezo mzuri na muhimu, licha ya matokeo ya sare naweza kusemma hatukuwa kwenye kiwango bora kwani tulipoteza nafasi tano za wazi za kufunga ambazo kama tungezitumia basi zingetuwezesha kupata ushindi mnono ugenini.
Kipindi cha pili tulicheza vizuri na kutengeneza nafasi nyingi, lakini huu ndio mpira wa miguu tunarudi nyumbani kujipanga na sitarajii kuona tunarudia makosa.”