Hatimaye Nahodha na Mshambuliaji wa klabu ya Arsenal ya England, Pierre Emerick Aubameyang amesaini mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia klabu hiyo yenye maskani yake makuu Kaskazini mwa jijini London.

Mshambuliaji huyo kutoka nchini Gabon amesaini mkataba mpya, baada ya kukamilisha mazungumzo na uongozi wa klabu hiyo, ambao ulionyesha kila sababu ya kutaka kuendelea kufanya kazi na nyota huyo, ambaye alisajiliwa klabuni hapo mwaka 2018, akitokea Borussia Dortmund chini ya utawala wa babu Arsene Wenger.

Aubameyang mwenye miaka 31 ataendelea kuwa sehemu ya kikosi cha Arsenal hadi mwaka 2023, baada ya kusaini dili hilo ambalo litamfanya awe analipwa mshahara wa Pauni 250,000 kwa juma.

Aubameyang amesema:”Mwisho wa siku nimesaini bonge moja ya saini, nina furaha kuwa ndani ya Arsenal.  Hapa ni nyumbani na ni furaha kwangu.

“Siku ya leo (jana) ni kubwa kwangu na ninahitaji kuwa Legend ndani ya Arsenal na nitakapoondoka niache alama. Ni muda wangu wa kazi na nitapambana.”

Kabla ya kusaini mkataba mpya jana Septemba 15, Aubameyang alihusishwa na taarifa za kuwaniwa na klabu za ndani na nje ya England, huku manguli wa Ligi ya nchini Hispania Real Madrid na FC Barcelona walikua wakitajwa mno na vyombo vya habari.

Pierre Emerick Aubameyang akiitazama jezi ya nahodha wa zamani wa Aresenal Thiery Henry, baada ya kusaini mkataba mpya, Septemba 15.
Pierre Emerick Aubameyang akiwa na baba yake mzazi ‘mzee Aubameyang’, baada ya kusaini mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia Arsenal, Septemba 15.
Pierre Emerick Aubameyang akionyesha jezi namba 14 ambayo anaitumia kwenye kikosi cha Arsenal. Baada ya kusaini mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia Arsenal, Septemba 15.
Pierre Emerick Aubameyang akiwa na meneja wa Arsenal Mikael Arteta, akionyesha ishara ya kusaini mkataba mpya, Septemba 15.

TANZIA: ACP Jonathan Shana afariki dunia
Chelsea yachomoza England