Baadhi ya Wanachama na Mashabiki wa Simba SC wameanza safari ya kuelekea Chalinze mkoani Pwani, tayari kwa uzinduzi wa Hamasa ya kuelekea mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Robo Fainali Ligi ya Mabingwa barani Afrika dhidi ya Wydad Casablanca.
Mchezo huo utachezwa Jumamosi (April 22), katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam kuanzia saa kumi jioni kwa saa za Tanzania.
Simba SC kupitia vyanzo vyake vya habari imethibitisha kuanza kwa safari hiyo eneo la Ubungo jijini Dar es salaam, kupitia Kibaha, Mlandizi hadi Chalinze,ikiongozwa na Meneja wa Habari na Mawasilino wa klabu hiyo Ahmed Ally.
Alipozungumza na Waandishi wa Habari jana Jumanne (April 18), Ahmed Ally alisema: “Furaha ya Wanasimba haijakamilika, wanatudai nusu fainali. Tunawaomba Wanasimba tushikamane, pamoja na ubora alionao Wydad lakini tukisimama kama Simba hakuna linaloshindikana.”
“Lazima tukawaadhibu Wydad, lazima tuwaonyeshe yaliyomo yamo. Itakuwa ni siku ya Eid siku hiyo, njoo umeshiba pilau lako, umewaka uje tuhakikishe Wydad wanakaa.”
“Kuhusu hamasa tumeshaanza, mara nyingi tunakuwa na uzinduzi, uzinduzi utafanyika kesho mkoani Pwani, wilaya ya Chalinze kwenye tawi la Wekundu wa Chamazi.”
“Kwa Wanasimba ambao wanataka kwenda Chalinze kwenye uzinduzi tutaondoka kutokea Ubungo sheli kesho saa 3 asubuhi. Tutasimama kidogo Mbezi Mwisho, Kibaha, Mlandizi alafu tunakwenda kufanya balaa Chalinze.”