Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, leo limeonesha nyumba ambayo bilionea Mohammed Dewji alifichwa baada ya kutekwa Oktoba 11 mwaka huu katika hoteli ya Colosseum jijini Dar es Salaam.
Akizungumza leo mbele ya waandishi wa habari akiwa katika nyumba hiyo ambayo iko Mbezi Beach, kilometa moja kutoka barabara ya Old Bagamoyo, Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Lazaro Mambosasa amesema kuwa nyumba hiyo imebainika kufuatia uchunguzi ulioendelea kufanywa na jeshi hilo hata baada ya Mo kupatikana.
Alisema kuwa nyumba hiyo ya Ghorofa moja ni ya Mzee Mwansasu lakini hivi sasa inamilikiwa na binti zake ambao waliipangisha.
Alifafanua kuwa wapangaji wa nyumba hiyo ambao ni raia wa kigeni walipitia kwa dereva taxi aitwaye Twalib Mussa ambaye alihusika kama dalali.
“Katika nyumba hii, walitokea watu ambao walijitambulisha kuwa ni wafanyabiashara wa madini kutoka Afrika Kusini, walipanga lakini walipitia kwa Twalib Mussa.
Alieleza kuwa walilipa kiasi cha $,1500 (sawa na Sh 3.4 milioni) kwa mwezi. Wahusika wa nyumba walipata kiasi cha $1,300 na Mussa ambaye alikuwa kama dalali alipata $200.
Naye Mussa ambaye alijitambulisha kuwa ni dereva Taxi wa eneo hilo, alikiri kuwapokea na kufanikisha upatikanaji wa nyumba kwa wageni hao.
Watu hao ambao bado hawajajulikana walimtelekeza Mo Dewji katika viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Salaam, baada ya kukaa naye kama mateka kwa siku tisa.